← Zephaniah (3/3) |
1. | Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! |
2. | Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini Bwana; hakumkaribia Mungu wake. |
3. | Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; makadhi wake ni mbwa-mwitu wa jioni; hawasazi kitu cho chote hata siku ya pili. |
4. | Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu. |
5. | Bwana kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya. |
6. | Nimekatilia mbali mataifa, buruji zao zina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko. |
7. | Nalisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote. |
8. | Basi ningojeni, asema Bwana, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu. |
9. | Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la Bwana, wamtumikie kwa nia moja. |
10. | Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. |
11. | Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. |
12. | Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana. |
13. | Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya. |
14. | Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. |
15. | Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena. |
16. | Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. |
17. | Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba. |
18. | Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao. |
19. | Tazama, wakati huo nitawapatiliza watu wote wanaokutesa; nami nitamponya yeye achechemeaye, nami nitamkusanya yeye aliyefukuzwa; nami nitawafanya kuwa sifa na jina, hao ambao fedheha yao ilikuwa katika dunia yote. |
20. | Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi kuwa sifa na jina, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema Bwana. |
← Zephaniah (3/3) |