Zephaniah (1/3) → |
1. | Neno la Bwana lililomjia Sefania, mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia; katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda. |
2. | Nitavikomesha kabisa vitu vyote, visionekane juu ya uso wa nchi, asema Bwana. |
3. | Nitamkomesha mwanadamu na mnyama; nitakomesha ndege wa angani, na samaki wa baharini, na hayo makwazo pamoja na wabaya; nami nitamkatilia mbali mwanadamu, asionekane juu ya uso wa nchi, asema Bwana. |
4. | Nami nitaunyosha mkono wangu juu ya Yuda, na juu ya watu wote wakaao Yerusalemu; nami nitayakatilia mbali mabaki ya Baali, yasionekane mahali hapa, na hilo jina la Wakemari pamoja na makuhani; |
5. | na wale walisujudiao jeshi la mbinguni juu ya dari za nyumba; na hao waabuduo, waapao kwa Bwana na kuapa pia kwa Malkamu; |
6. | na hao waliorudi nyuma, na kuacha kumfuata Bwana; na hao wasiomtafuta Bwana, wala kumwulizia. |
7. | Nyamaza kimya mbele za Bwana MUNGU; Kwa maana siku ya Bwana i karibu; Kwa kuwa Bwana ameweka tayari dhabihu, Amewatakasa wageni wake. |
8. | Na itakuwa, katika siku ile ya dhabihu ya Bwana, nitawaadhibu wakuu, na wana wa mfalme, na watu wote waliovaa mavazi ya kigeni. |
9. | Na katika siku ile nitawaadhibu hao wote warukao juu ya kizingiti, waijazao nyumba ya bwana wao udhalimu na udanganyifu. |
10. | Na katika siku ile, asema Bwana kutakuwako sauti ya kilio kutoka lango la samaki, na mlio mkuu katika mtaa wa pili, na mshindo mkuu kutoka milimani. |
11. | Haya! Lieni, ninyi mkaao katika Makteshi, maana wafanya biashara wote wameangamia; hao wote waliokuwa na mizigo ya fedha wamekatiliwa mbali. |
12. | Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, Bwana hatatenda mema, wala hatatenda mabaya. |
13. | Na huko utajiri wao utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa; naam, watajenga nyumba, lakini hawatakaa ndani yake; nao watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake. |
14. | Hiyo siku ya Bwana iliyo kuu i karibu; I karibu, nayo inafanya haraka sana; Naam, sauti ya siku ya Bwana; Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko! |
15. | Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu, |
16. | Siku ya tarumbeta na ya kamsa, Juu ya miji yenye maboma, Juu ya buruji zilizo ndefu sana. |
17. | Nami nitawaletea wanadamu dhiki, hata watakwenda kama vipofu, kwa sababu wamemtenda Bwana dhambi; na damu yao itamwagwa kama mavumbi, na nyama yao kama mavi. |
18. | Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya Bwana; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha. |
Zephaniah (1/3) → |