← Zechariah (9/14) → |
1. | Ufunuo wa neno la Bwana, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea Bwana; |
2. | na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi. |
3. | Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu. |
4. | Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto. |
5. | Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu. |
6. | Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti. |
7. | Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi. |
8. | Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu. |
9. | Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. |
10. | Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia. |
11. | Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. |
12. | Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu. |
13. | Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa. |
14. | Naye Bwana ataonekana juu yao, Na mshale wake utatoka kama umeme; Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta, Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini. |
15. | Bwana wa majeshi atawalinda; Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo; Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai; Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu. |
16. | Na Bwana, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimeta-meta juu ya nchi yake. |
17. | Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi! Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi! Nafaka itawasitawisha vijana wanaume, Na divai mpya vijana wanawake. |
← Zechariah (9/14) → |