← Zechariah (14/14) |
1. | Tazama, siku moja ya Bwana inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako. |
2. | Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali. |
3. | Hapo ndipo atakapotokea Bwana, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita. |
4. | Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini. |
5. | Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku za Uzia, mfalme wa Yuda; na Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye. |
6. | Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi; |
7. | lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na Bwana; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru. |
8. | Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba maji yaliyo hai yatatoka katika Yerusalemu; nusu yake itakwenda upande wa bahari ya mashariki, na nusu yake upande wa bahari ya magharibi; wakati wa hari na wakati wa baridi itakuwa hivi. |
9. | Naye Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa mmoja, na jina lake moja. |
10. | Nchi yote itageuzwa kuwa kama Araba, toka Geba mpaka Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu; naye atainuliwa juu, atakaa mahali pake mwenyewe, toka lango la Benyamini mpaka mahali pa lango la kwanza, mpaka lango la pembeni; tena toka mnara wa Hananeli mpaka mashinikizo ya mfalme. |
11. | Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena; lakini Yerusalemu utakaa salama. |
12. | Na hii ndiyo tauni, ambayo Bwana atawapiga watu wote waliofanya vita juu ya Yerusalemu; nyama ya mwili wao itaharibika, wasimamapo juu ya miguu yao, na macho yao yataharibika ndani ya vichwa vyao, na ndimi zao zitaharibika vinywani mwao. |
13. | Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba mashaka makubwa yatokayo kwa Bwana yatakuwa kati yao; na kila mmoja wao atakamata mkono wa jirani yake, na mkono wake utainuliwa ili kushindana na mkono wa jirani yake. |
14. | Yuda naye atafanya vita juu ya Yerusalemu; na huo utajiri wa mataifa wa pande zote utakusanyika, dhahabu, na fedha, na mavazi; vitu vingi sana. |
15. | Na hivyo ndivyo itakavyokuwa tauni ya farasi, na nyumbu, na ngamia, na punda, na ya hao wanyama wote watakaokuwamo matuoni mle, kama tauni hiyo. |
16. | Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, na kuishika sikukuu ya Vibanda. |
17. | Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, mvua haitanyesha kwao. |
18. | Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo Bwana atawapiga mataifa, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda. |
19. | Hii ndiyo adhabu ya Misri, na adhabu ya mataifa yote, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda. |
20. | Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA Bwana; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya Bwana vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. |
21. | Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa Bwana wa majeshi; nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake; wala siku hiyo hatakuwamo tena mfanya biashara ndani ya nyumba ya Bwana wa majeshi. |
← Zechariah (14/14) |