← SongOfSongs (8/8) |
1. | Laiti ungekuwa kama ndugu yangu, Aliyeyanyonya matiti ya mamangu! Kama ningekukuta huko nje, Ningekubusu, asinidharau mtu. |
2. | Ningekuongoza nyumbani mwa mamangu, Naye angenifundisha; |
3. | Mkono wake wa kushoto ungekuwa chini ya kichwa changu, Nao wa kuume ungenikumbatia. |
4. | Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwani kuyachochea mapenzi, au kuyaamsha, Hata yatakapoona vema? |
5. | Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani, Akimtegemea mpendwa wake? Nalikuamsha chini ya huo mpera; Huko mama yako alikuonea utungu, Aliona utungu aliyekuzaa. |
6. | Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu. |
7. | Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha; Kama mtu angetoa badala ya upendo Mali yote ya nyumbani mwake, Angedharauliwa kabisa. |
8. | Kwetu sisi tuna umbu mdogo, Wala hana maziwa; Tumfanyieje umbu letu, Siku atakapoposwa? |
9. | Kama akiwa tu ukuta, Tumjengee buruji za fedha; Na kama akiwa ni mlango, Tumhifadhi kwa mbao za mierezi. |
10. | Mimi nalikuwa ukuta, Na maziwa yangu kama minara; Ndipo nikawa machoni pake Kama mtu aliyeipata amani. |
11. | Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-hamomi Akawakodisha walinzi hilo shamba lake la mizabibu; Kila mtu atoe vipande elfu vya fedha kwa matunda yake. |
12. | Shamba langu la mizabibu, lililo langu mimi, li mbele yangu. Basi, Sulemani, wewe uwe na elfu zako, Na hao wayalindao matunda yake wapewe mia mbili. |
13. | Wewe ukaaye bustanini, Hao rafiki huisikiliza sauti yako; Unisikizishe mimi. |
14. | Ukimbie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya manukato. |
← SongOfSongs (8/8) |