| SongOfSongs (1/8) → |
| 1. | Wimbo ulio bora, wa Sulemani. |
| 2. | Kubusu na anibusu kwa kinywa chake. Maana pambaja zako zapita divai; |
| 3. | Manukato yako yanukia vizuri; Jina lako ni kama marhamu iliyomiminwa; Kwa hiyo wanawali hukupenda. |
| 4. | Nivute nyuma yako, na tukimbie; Mfalme ameniingiza vyumbani mwake. Tutafurahi na kukushangilia; Tutazinena pambaja zako kuliko divai; Ndiyo, ina haki wakupende. |
| 5. | Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Enyi binti za Yerusalemu, Mfano wa hema za Kedari, Kama mapazia yake Sulemani. |
| 6. | Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, Kwa sababu jua limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda. |
| 7. | Nijulishe, ee mpendwa wa nafsi yangu, Ni wapi utakapolisha kundi lako, Ni wapi utakapolilaza adhuhuri. Kwa nini niwe kama aliyefungiwa kidoto, Karibu na makundi ya wenzako? |
| 8. | Usipojua, wewe uliye mzuri katika wanawake, Shika njia uzifuate nyayo za kondoo, Na kuwalisha wana-mbuzi wako Karibu na hema za wachungaji. |
| 9. | Mpenzi wangu, nimekulinganisha Na farasi katika magari ya Farao. |
| 10. | Mashavu yako ni mazuri kwa mashada, Shingo yako kwa mikufu ya vito. |
| 11. | Tutakufanyizia mashada ya dhahabu, Yenye vifungo vya fedha. |
| 12. | Muda mfalme alipoketi juu ya matakia, Nardo yangu ilitoa harufu yake. |
| 13. | Mpendwa wangu ni kama mfuko wa manemane Ukilazwa usiku maziwani mwangu. |
| 14. | Mpendwa wangu ni kama kishada cha hina, Katika mizabibu huko Engedi. |
| 15. | Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua. |
| 16. | Tazama, u mzuri, mpendwa wangu, Wapendeza, na kitanda chetu ni majani; |
| 17. | Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi. |
| SongOfSongs (1/8) → |