← Romans (4/16) → |
1. | Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? |
2. | Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. |
3. | Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. |
4. | Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. |
5. | Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. |
6. | Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, |
7. | Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. |
8. | Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi. |
9. | Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. |
10. | Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. |
11. | Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; |
12. | tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa. |
13. | Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. |
14. | Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika. |
15. | Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa. |
16. | Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; |
17. | (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. |
18. | Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. |
19. | Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara. |
20. | Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; |
21. | huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. |
22. | Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki. |
23. | Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; |
24. | bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; |
25. | ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki. |
← Romans (4/16) → |