← Romans (2/16) → |
1. | Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. |
2. | Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. |
3. | Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? |
4. | Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? |
5. | Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, |
6. | atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; |
7. | wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; |
8. | na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu; |
9. | dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia; |
10. | bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; |
11. | kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu. |
12. | Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria. |
13. | Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. |
14. | Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. |
15. | Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; |
16. | katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu. |
17. | Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, |
18. | na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, |
19. | na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, |
20. | mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati; |
21. | basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? |
22. | Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? |
23. | Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati? |
24. | Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa. |
25. | Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. |
26. | Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa? |
27. | Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaihalifu torati? |
28. | Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili; |
29. | bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu. |
← Romans (2/16) → |