← Romans (13/16) → |
1. | Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. |
2. | Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. |
3. | Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake; |
4. | kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu. |
5. | Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri. |
6. | Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo. |
7. | Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima. |
8. | Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. |
9. | Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. |
10. | Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria. |
11. | Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini |
12. | Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. |
13. | Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. |
14. | Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake. |
← Romans (13/16) → |