Romans (1/16) → |
1. | Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; |
2. | ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; |
3. | yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, |
4. | na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; |
5. | ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; |
6. | ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; |
7. | kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. |
8. | Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima. |
9. | Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, |
10. | siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu. |
11. | Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara; |
12. | yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu. |
13. | Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nalikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa hata sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine. |
14. | Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. |
15. | Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi. |
16. | Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. |
17. | Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. |
18. | Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. |
19. | Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. |
20. | Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; |
21. | kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. |
22. | Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; |
23. | wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. |
24. | Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. |
25. | Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. |
26. | Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; |
27. | wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. |
28. | Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. |
29. | Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, |
30. | wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, |
31. | wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; |
32. | ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao. |
Romans (1/16) → |