← Psalms (99/150) → |
1. | Bwana ametamalaki, mataifa wanatetemeka; Ameketi juu ya makerubi, nchi inatikisika. |
2. | Bwana katika Sayuni ni mkuu, Naye ametukuka juu ya mataifa yote. |
3. | Na walishukuru jina lake kuu la kuhofiwa; Ndiye mtakatifu. |
4. | Nguvu za mfalme nazo zapenda hukumu; Wewe ndiwe uliyeithibitisha adili; Ulifanya hukumu na haki katika Yakobo. |
5. | Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni penye kiti cha miguu yake; Ndiye mtakatifu. |
6. | Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia; |
7. | Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao. Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa. |
8. | Ee Bwana, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu; Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe Ingawa uliwapatiliza matendo yao. |
9. | Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu. |
← Psalms (99/150) → |