← Psalms (119/150) → |
1. | Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana. |
2. | Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote. |
3. | Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake. |
4. | Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana. |
5. | Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako. |
6. | Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote. |
7. | Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako |
8. | Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa |
9. | Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. |
10. | Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako. |
11. | Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. |
12. | Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako. |
13. | Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako. |
14. | Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi. |
15. | Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako. |
16. | Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako. |
17. | Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. |
18. | Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. |
19. | Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. |
20. | Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. |
21. | Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. |
22. | Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. |
23. | Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. |
24. | Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. |
25. | Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako. |
26. | Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. |
27. | Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. |
28. | Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. |
29. | Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. |
30. | Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. |
31. | Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe. |
32. | Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu. |
33. | Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho. |
34. | Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. |
35. | Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo. |
36. | Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. |
37. | Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. |
38. | Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako. |
39. | Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. |
40. | Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. |
41. | Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako. |
42. | Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako. |
43. | Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. |
44. | Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. |
45. | Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. |
46. | Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. |
47. | Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. |
48. | Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako. |
49. | Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha. |
50. | Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha. |
51. | Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako. |
52. | Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji. |
53. | Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako. |
54. | Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu. |
55. | Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako. |
56. | Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako. |
57. | Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake. |
58. | Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako. |
59. | Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako. |
60. | Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako. |
61. | Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako. |
62. | Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki. |
63. | Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako. |
64. | Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako. |
65. | Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako. |
66. | Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako. |
67. | Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako. |
68. | Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako. |
69. | Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako. |
70. | Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako. |
71. | Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako. |
72. | Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha. |
73. | Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako. |
74. | Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako. |
75. | Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa. |
76. | Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. |
77. | Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu. |
78. | Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako. |
79. | Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako. |
80. | Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika. |
81. | Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako. |
82. | Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji? |
83. | Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako. |
84. | Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia? |
85. | Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako. |
86. | Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie. |
87. | Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako. |
88. | Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako. |
89. | Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele. |
90. | Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa. |
91. | Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako. |
92. | Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu. |
93. | Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha. |
94. | Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako. |
95. | Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako. |
96. | Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno. |
97. | Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa. |
98. | Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote. |
99. | Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo. |
100. | Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako. |
101. | Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako. |
102. | Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha. |
103. | Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu. |
104. | Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo. |
105. | Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. |
106. | Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako. |
107. | Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako. |
108. | Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako. |
109. | Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau. |
110. | Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako. |
111. | Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu. |
112. | Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele. |
113. | Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda. |
114. | Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea. |
115. | Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu. |
116. | Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu. |
117. | Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima. |
118. | Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo. |
119. | Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako. |
120. | Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako. |
121. | Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea. |
122. | Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee. |
123. | Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako. |
124. | Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe. |
125. | Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako. |
126. | Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako. |
127. | Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi. |
128. | Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia. |
129. | Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika. |
130. | Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga. |
131. | Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako. |
132. | Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako. |
133. | Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki. |
134. | Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako. |
135. | Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako. |
136. | Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako. |
137. | Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili. |
138. | Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi. |
139. | Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako. |
140. | Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda. |
141. | Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako. |
142. | Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli. |
143. | Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu. |
144. | Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi. |
145. | Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako. |
146. | Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako. |
147. | Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini. |
148. | Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako. |
149. | Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako. |
150. | Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako. |
151. | Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli. |
152. | Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele. |
153. | Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako. |
154. | Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako. |
155. | Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako. |
156. | Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako. |
157. | Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako. |
158. | Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako. |
159. | Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako. |
160. | Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele. |
161. | Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako. |
162. | Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi. |
163. | Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda. |
164. | Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako. |
165. | Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza. |
166. | Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda. |
167. | Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno. |
168. | Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako. |
169. | Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako. |
170. | Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako. |
171. | Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako. |
172. | Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki. |
173. | Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako. |
174. | Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu. |
175. | Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie. |
176. | Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako. |
← Psalms (119/150) → |