← Psalms (118/150) → |
1. | Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. |
2. | Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. |
3. | Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. |
4. | Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. |
5. | Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi. |
6. | Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? |
7. | Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. |
8. | Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu. |
9. | Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu. |
10. | Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. |
11. | Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. |
12. | Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. |
13. | Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia. |
14. | Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu. |
15. | Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu. |
16. | Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu. |
17. | Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. |
18. | Bwana ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife. |
19. | Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru Bwana. |
20. | Lango hili ni la Bwana, Wenye haki ndio watakaoliingia. |
21. | Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu. |
22. | Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni. |
23. | Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu. |
24. | Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia. |
25. | Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi. |
26. | Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana. |
27. | Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu. |
28. | Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza. |
29. | Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. |
← Psalms (118/150) → |