← Psalms (106/150) → |
1. | Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. |
2. | Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana, Kuzihubiri sifa zake zote? |
3. | Heri washikao hukumu, Na kutenda haki sikuzote. |
4. | Ee Bwana, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. Unijilie kwa wokovu wako, |
5. | Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako. |
6. | Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu, Tumetenda maovu, tumefanya ubaya. |
7. | Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu. |
8. | Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu. |
9. | Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda. |
10. | Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao. |
11. | Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao. |
12. | Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake. |
13. | Wakayasahau matendo yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake. |
14. | Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani. |
15. | Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao. |
16. | Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa Bwana. |
17. | Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu. |
18. | Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya. |
19. | Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka. |
20. | Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani. |
21. | Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri. |
22. | Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. |
23. | Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. |
24. | Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake. |
25. | Bali wakanung'unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya Bwana. |
26. | Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani, |
27. | Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali. |
28. | Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu. |
29. | Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia. |
30. | Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa. |
31. | Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele. |
32. | Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, |
33. | Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake. |
34. | Hawakuwaharibu watu wa nchi Kama Bwana alivyowaambia; |
35. | Bali walijichanganya na mataifa, Wakajifunza matendo yao. |
36. | Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao. |
37. | Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. |
38. | Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu. |
39. | Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao. |
40. | Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake. |
41. | Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala. |
42. | Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao. |
43. | Mara nyingi aliwaponya, Bali walikuwa wakimwasi kwa mashauri yao, Wakadhilika katika uovu wao. |
44. | Lakini aliyaangalia mateso yao, Aliposikia kilio chao. |
45. | Akawakumbukia agano lake; Akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake; |
46. | Akawajalia kuhurumiwa Na watu wote waliowateka. |
47. | Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako. |
48. | Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Watu wote na waseme, Amina. Haleluya. |
← Psalms (106/150) → |