← Psalms (105/150) → |
1. | Haleluya. |
2. | Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote. |
3. | Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. |
4. | Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote. |
5. | Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya, Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. |
6. | Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. |
7. | Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. |
8. | Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. |
9. | Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka. |
10. | Alilomthibitishia Yakobo liwe amri, Na Israeli liwe agano la milele. |
11. | Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa. |
12. | Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa, Naam, watu wachache na wageni ndani yake, |
13. | Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine. |
14. | Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. |
15. | Akisema, Msiwaguse masihi |
16. | Akaiita njaa iijilie nchi, Akakiharibu chakula chote walichokitegemea. |
17. | Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani. |
18. | Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma. |
19. | Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya Bwana ilimjaribu. |
20. | Mfalme alituma watu akamfungua, Mkuu wa watu akamwachia. |
21. | Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake, Na mwenye amri juu ya mali zake zote. |
22. | Awafunge masheki wake kama apendavyo, Na kuwafundisha wazee wake hekima. |
23. | Israeli naye akaingia Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu. |
24. | Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao. |
25. | Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake. |
26. | Akamtuma Musa, mtumishi wake, Na Haruni ambaye amemchagua. |
27. | Akaweka mambo ya ishara zake kati yao, Na miujiza katika nchi ya Hamu. |
28. | Alituma giza, kukafunga giza, Wala hawakuyaasi maneno yake. |
29. | Aliyageuza maji yao yakawa damu, Akawafisha samaki wao. |
30. | Nchi yao ilijaa vyura, Vyumbani mwa wafalme wao. |
31. | Alisema, kukaja makundi ya mainzi, Na chawa mipakani mwao mwote. |
32. | Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe, Na moto wa miali katika nchi yao. |
33. | Akaipiga mizabibu yao na mitini yao, Akaivunja miti ya mipaka yao. |
34. | Alisema, kukaja nzige, Na tunutu wasiohesabika; |
35. | Wakaila miche yote ya nchi yao, Wakayala matunda ya ardhi yao. |
36. | Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi, Malimbuko ya nguvu zao. |
37. | Akawatoa hali wana fedha na dhahabu, Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa. |
38. | Misri ilifurahi walipoondoka, Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia. |
39. | Alitandaza wingu liwe funiko, Na moto utoe nuru usiku. |
40. | Walipotaka akaleta kware, Akawashibisha chakula cha mbinguni. |
41. | Akaufunua mwamba, kukabubujika maji, Yakapita pakavuni kama mto. |
42. | Maana alilikumbuka neno lake takatifu, Na Ibrahimu, mtumishi wake. |
43. | Akawatoa watu wake kwa shangwe, Na wateule wake kwa nyimbo za furaha. |
44. | Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu; |
45. | Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake. Haleluya. |
← Psalms (105/150) → |