← Psalms (104/150) → |
1. | Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama. |
2. | Umejivika nuru kama vazi; Umezitandika mbingu kama pazia; |
3. | Na kuziweka nguzo za orofa zake majini. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, Na kwenda juu ya mabawa ya upepo, |
4. | Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali. |
5. | Uliiweka nchi juu ya misingi yake, Isitikisike milele. |
6. | Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi, Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. |
7. | Kwa kukemea kwako yakakimbia, Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi, |
8. | Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, Mpaka mahali ulipoyatengenezea. |
9. | Umeweka mpaka yasiupite, Wala yasirudi kuifunikiza nchi. |
10. | Hupeleka chemchemi katika mabonde; Zapita kati ya milima; |
11. | Zamnywesha kila mnyama wa kondeni; Punda mwitu huzima kiu yao. |
12. | Kandokando hukaa ndege wa angani; Kati ya matawi hutoa sauti zao. |
13. | Huinywesha milima toka orofa zake; Nchi imeshiba mazao ya kazi zako. |
14. | Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi, |
15. | Na divai imfurahishe mtu moyo wake. Aung'aze uso wake kwa mafuta, Na mkate umburudishe mtu moyo wake. |
16. | Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda. |
17. | Ndimo ndege wafanyamo vitundu vyao, Na korongo, misunobari ni nyumba yake. |
18. | Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu, Na magenge ni kimbilio la wibari. |
19. | Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati, Jua latambua kuchwa kwake. |
20. | Wewe hufanya giza, kukawa usiku, Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu. |
21. | Wana-simba hunguruma wakitaka mawindo, Ili kutafuta chakula chao kwa Mungu. |
22. | Jua lachomoza, wanakwenda zao, Na kujilaza mapangoni mwao. |
23. | Mwanadamu atoka kwenda zake kazini, Na kwenye utumishi wake mpaka jioni. |
24. | Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako. |
25. | Bahari iko kule, kubwa na upana, Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika, Viumbe hai vidogo kwa vikubwa. |
26. | Ndimo zipitamo merikebu, Ndimo alimo lewiathani uliyemwumba acheze humo. |
27. | Hao wote wanakungoja Wewe, Uwape chakula chao kwa wakati wake. |
28. | Wewe huwapa, Wao wanakiokota; Wewe waukunjua mkono wako, Wao wanashiba mema; |
29. | Wewe wauficha uso wako, Wao wanafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao, |
30. | Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi. |
31. | Utukufu wa Bwana na udumu milele; Bwana na ayafurahie matendo yake. |
32. | Aitazama nchi, inatetemeka; Aigusa milima, inatoka moshi. |
33. | Nitamwimbia Bwana maadamu ninaishi; Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai; |
34. | Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia Bwana. |
35. | Wenye dhambi waangamizwe katika nchi, Watendao ubaya wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. |
← Psalms (104/150) → |