← Psalms (103/150) → |
1. | Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. |
2. | Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. |
3. | Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, |
4. | Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, |
5. | Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai; |
6. | Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa. |
7. | Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake. |
8. | Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. |
9. | Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. |
10. | Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. |
11. | Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. |
12. | Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. |
13. | Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. |
14. | Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi. |
15. | Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo. |
16. | Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena. |
17. | Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana; |
18. | Maana, wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye. |
19. | Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote. |
20. | Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake. |
21. | Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake. |
22. | Mhimidini Bwana, enyi matendo yake yote, Mahali pote pa milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. |
← Psalms (103/150) → |