← Psalms (102/150) → |
1. | Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie. |
2. | Usinifiche uso wako siku ya shida yangu, Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi. |
3. | Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga. |
4. | Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka, Naam, ninasahau kula chakula changu. |
5. | Kwa ajili ya sauti ya kuugua kwangu Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu. |
6. | Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani, Na kufanana na bundi wa mahameni. |
7. | Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro Aliye peke yake juu ya nyumba. |
8. | Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu Huapa kwa kunitaja mimi. |
9. | Maana nimekula majivu kama chakula, Na kukichanganya kinywaji changu na machozi. |
10. | Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako; Maana umeniinua na kunitupilia mbali. |
11. | Siku zangu zi kama kivuli kilichotandaa, Nami ninanyauka kama majani. |
12. | Bali Wewe, Bwana utaketi ukimiliki milele, Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi. |
13. | Wewe mwenyewe utasimama, Na kuirehemu Sayuni, Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia, Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia. |
14. | Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake, Na kuyaonea huruma mavumbi yake. |
15. | Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana, Na wafalme wote wa dunia utukufu wako; |
16. | Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, Atakapoonekana katika utukufu wake, |
17. | Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao. |
18. | Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo, Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana. |
19. | Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi, |
20. | Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa. |
21. | Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni, Na sifa zake katika Yerusalemu, |
22. | Pindi mataifa watapokusanyika pamoja, Falme nazo ili kumtumikia Bwana. |
23. | Amezipunguza nguvu zangu njiani; Amezifupisha siku zangu. |
24. | Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi. |
25. | Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako. |
26. | Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika. |
27. | Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma. |
28. | Wana wa watumishi wako watakaa, Na wazao wao wataimarishwa mbele zako. |
← Psalms (102/150) → |