← Numbers (16/36) → |
1. | Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; |
2. | nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; |
3. | nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana? |
4. | Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; |
5. | kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. |
6. | Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; |
7. | vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za Bwana kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu Bwana atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi. |
8. | Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; |
9. | Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; |
10. | tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? |
11. | Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia? |
12. | Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; |
13. | je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? |
14. | Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. |
15. | Musa akakasirika sana, akamwambia Bwana. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. |
16. | Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya Bwana kesho, wewe, na wao, na Haruni; |
17. | mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za Bwana, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. |
18. | Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. |
19. | Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa Bwana ukatokea mbele ya mkutano wote. |
20. | Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, |
21. | Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja. |
22. | Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote? |
23. | Bwana akasema na Musa, na kumwambia, |
24. | Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu. |
25. | Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye. |
26. | Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. |
27. | Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. |
28. | Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. |
29. | Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. |
30. | Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana |
31. | Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; |
32. | nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. |
33. | Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. |
34. | Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. |
35. | Kisha moto ukatoka kwa Bwana, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba. |
36. | Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, |
37. | Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu; |
38. | vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuzihasiri nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za Bwana, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli. |
39. | Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu; |
40. | viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni awaye yote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za Bwana; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama Bwana alivyonena naye, kwa mkono wa Musa. |
41. | Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung'unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa Bwana. |
42. | Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa Bwana ukaonekana. |
43. | Na Musa na Haruni wakaenda hapo mbele ya hema ya kukutania. |
44. | Naye Bwana akanena na Musa, na kumwambia, |
45. | Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi. |
46. | Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa Bwana; hiyo tauni imeanza. |
47. | Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. |
48. | Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. |
49. | Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. |
50. | Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa. |
← Numbers (16/36) → |