← Numbers (14/36) → |
1. | Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. |
2. | Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. |
3. | Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? |
4. | Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. |
5. | Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. |
6. | Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; |
7. | wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. |
8. | Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. |
9. | Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope. |
10. | Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote. |
11. | Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao. |
12. | Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao. |
13. | Basi Musa akamwambia Bwana, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao; |
14. | kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe Bwana u kati ya watu hawa; maana, wewe Bwana waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku. |
15. | Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema, |
16. | Ni kwa sababu yeye Bwana hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani. |
17. | Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema, |
18. | Bwana ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne. |
19. | Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. |
20. | Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa; |
21. | lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa Bwana; |
22. | kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; |
23. | hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; |
24. | lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki. |
25. | Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu. |
26. | Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, |
27. | Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hata lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo. |
28. | Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; |
29. | mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia, |
30. | hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. |
31. | Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa. |
32. | Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili. |
33. | Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani. |
34. | Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu. |
35. | Mimi Bwana nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko Watakakokufa. |
36. | Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi, |
37. | watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya Bwana. |
38. | Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi. |
39. | Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaombolea sana. |
40. | Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali Bwana alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi. |
41. | Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyahalifu maagizo ya Bwana? Maana halitafanikiwa jambo hilo. |
42. | Msikwee, kwa kuwa Bwana hamo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu. |
43. | Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimwandame Bwana, kwa hiyo Bwana hatakuwa pamoja nanyi. |
44. | Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la agano la Bwana halikutoka humo maragoni, wala Musa hakutoka. |
45. | Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakatelemka, wakawapiga na kuwaangusha, hata kufikilia Horma. |
← Numbers (14/36) → |