← Numbers (11/36) → |
1. | Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. |
2. | Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma. |
3. | Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao. |
4. | Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule? |
5. | Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; |
6. | lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. |
7. | Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. |
8. | Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. |
9. | Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. |
10. | Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika. |
11. | Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? |
12. | Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? |
13. | Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. |
14. | Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. |
15. | Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu. |
16. | Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. |
17. | Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako. |
18. | Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula. |
19. | Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini; |
20. | lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani? |
21. | Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima. |
22. | Je! Makundi ya kondoo na ng'ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha? |
23. | Bwana akamwambia Musa, Je! Mkono wa Bwana umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo. |
24. | Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya Bwana; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema. |
25. | Ndipo Bwana akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. |
26. | Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini. |
27. | Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. |
28. | Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. |
29. | Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake. |
30. | Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli. |
31. | Kisha upepo ukavuma kutoka kwa Bwana, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi. |
32. | Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote. |
33. | Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za Bwana ziliwaka juu ya watu, Bwana akawapiga watu kwa pigo kuu mno. |
34. | Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani. |
35. | Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi. |
← Numbers (11/36) → |