← Nehemiah (8/13) → |
1. | Na watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha torati ya Musa, Bwana aliyowaamuru Israeli. |
2. | Naye Ezra, kuhani, akaileta torati mbele ya kusanyiko, la wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza na mwezi wa saba. |
3. | Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha torati. |
4. | Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu. |
5. | Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; |
6. | Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi. |
7. | Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. |
8. | Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa. |
9. | Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. |
10. | Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu. |
11. | Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike. |
12. | Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa. |
13. | Hata siku ya pili wakuu wa mbari za mababa za watu wote, na makuhani, na Walawi, wakamkusanyikia Ezra, mwandishi, ili wapate kuyasikiliza maneno ya torati. |
14. | Wakaona ya kuwa imeandikwa katika torati, jinsi Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa, ya kwamba wana wa Israeli wakae katika vibanda, katika sikukuu ya mwezi wa saba; |
15. | na ya kwamba wahubiri na kutangaza katika miji yao yote, na katika Yerusalemu, kusema, Enendeni mlimani, mkalete matawi ya mzeituni, na matawi ya mzeituni-mwitu, na matawi ya mihadasi, na matawi ya mitende, na matawi ya miti minene, ili kufanya vibanda, kama ilivyoandikwa. |
16. | Basi watu wote wakatoka, wakayaleta, wakajifanyizia vibanda, kila mtu juu ya dari ya nyumba yake, na katika nyua zao, na katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja wa lango la maji, na katika uwanja wa lango la Efraimu. |
17. | Na mkutano wote wa watu, waliorudi kutoka nchi ya uhamisho wao, wakafanyiza vibanda, wakakaa katika vibanda hivyo; maana tokea siku za Yoshua, mwana wa Nuni, hata siku ile, wana wa Israeli hawakufanya hivyo. Pakawa na furaha kubwa sana. |
18. | Tena siku baada ya siku, tangu siku ya kwanza hata siku ya mwisho, akasoma katika kitabu cha torati ya Mungu. Wakafanya sikukuu muda wa siku saba; na siku ya nane palikuwa na kusanyiko la makini, kama ilivyoagizwa. |
← Nehemiah (8/13) → |