← Nahum (2/3) → |
1. | Yeye asetaye vipande vipande amepanda juu mbele ya uso wako; zishike silaha, ilinde njia, vitie nguvu viuno vyako, uongeze uwezo wako sana. |
2. | Kwa maana Bwana anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao. |
3. | Ngao ya mashujaa wake imefanywa kuwa nyekundu, watu walio hodari wa vita wamevaa nguo nyekundu sana; magari ya vita yametameta kwa chuma cha pua siku ya kujitengeza kwake, na mikuki inatikiswa kwa namna ya kutisha. |
4. | Magari ya vita yanafanya mshindo njiani, Yanasongana-songana katika njia kuu; Kuonekana kwake ni kama mienge, Yanakwenda upesi kama umeme. |
5. | Awakumbuka watu wake wenye heshima; Wanajikwaa katika mwendo wao; Wanafanya haraka waende ukutani; Nacho kitu cha kuwafunika kimewekwa tayari. |
6. | Malango ya mito yamefunguka, na jumba la mfalme limeyeyushwa. |
7. | Husabu naye amefunuliwa, anachukuliwa, na wajakazi wake wanalia kama kwa sauti ya hua, wakipiga-piga vifua vyao. |
8. | Lakini Ninawi tokea zamani amekuwa kama ziwa la maji; ila hata sasa wanakimbia; Simameni! Simameni! Lakini hapana hata mmoja atazamaye nyuma. |
9. | Chukueni nyara za fedha; Chukueni nyara za dhahabu; Kwa maana ni akiba isiyoisha, Fahari ya vyombo vipendezavyo. |
10. | Amekuwa utupu, na ukiwa, na uharibifu; hata moyo unayeyuka, na magoti yanagongana-gongana; viunoni mwote mna utungu, na nyuso za wote zimekuwa nyeupe kwa hofu. |
11. | Kao la simba li wapi? Na mahali walishapo wana-simba pa wapi, mahali walipotembea simba mume na simba mke na mwana-simba, wala hapana aliyewatia hofu? |
12. | Simba alirarua vipande vipande chakula cha kuwatosha watoto wake, aliwasongea wake zake nyama, aliyajaza mapango yake mateka, na makao yake aliyajaza mawindo. |
13. | Tazama, mimi ni juu yako, asema Bwana wa majeshi, nami nitayateketeza magari yako ya vita katika moshi, na upanga utawala wana-simba wako; nami nitayakatilia mbali mawindo yako katika nchi, na sauti za wajumbe wako hazitasikiwa tena kamwe. |
← Nahum (2/3) → |