Nahum (1/3) → |
1. | Ufunuo juu ya Ninawi. Kitabu cha maono aliyoyaona Nahumu, Mwelkoshi. |
2. | Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; Bwana hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira. |
3. | Bwana si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; Bwana ana njia yake katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake. |
4. | Yeye huikemea bahari na kuikausha, pia huikausha mito yote; Bashani hulegea, na Karmeli; hulegea nalo ua la Lebanoni. |
5. | Milima hutetema mbele zake, navyo vilima huyeyuka; nayo dunia huinuliwa mbele za uso wake, naam, dunia na wote wakaao ndani yake. |
6. | Ni nani awezaye kusimama mbele za ghadhabu yake, naye ni nani awezaye kukaa katika ukali wa hasira yake? Hasira yake kali humwagwa kama moto, nayo majabali yapasuliwa na yeye. |
7. | Bwana ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao. |
8. | Lakini kwa gharika ifurikayo atapakomesha kabisa mahali pake, na kuwafuatia adui zake hata gizani. |
9. | Mnawaza nini juu ya Bwana? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili. |
10. | Kwa maana wangawa kama miiba iliyotatana, na kunyweshwa kana kwamba ni katika kunywa kwao, wataliwa kabisa kama mabua makavu. |
11. | Ametoka mmoja kwako, aniaye mabaya juu ya Bwana, atoaye mashauri yasiyofaa kitu. |
12. | Bwana asema hivi, Ijapokuwa wana nguvu zilizo timilifu, ijapokuwa ni wengi, hata hivyo watakatwa, naye atapita na kwenda zake. Ingawa nimekutesa, sitakutesa tena. |
13. | Na sasa nitakuvunjia nira yake, nami nitakupasulia mafungo yako. |
14. | Tena Bwana ametoa amri katika habari zako, ya kwamba asipandwe tena mtu awaye yote mwenye jina lako; toka nyumba ya miungu yako nitakatilia mbali sanamu ya kuchora, na sanamu ya kuyeyusha; nitakufanyia kaburi lako; kwa maana u mbovu. |
15. | Tazama, juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali. |
Nahum (1/3) → |