← Micah (7/7) |
1. | Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa hari, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. |
2. | Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. |
3. | Mikono yao inayashika mabaya wayatende kwa bidii; mtu mkuu aomba rushwa, kadhi yu tayari kuipokea; mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. |
4. | Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. |
5. | Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. |
6. | Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. |
7. | Lakini mimi, nitamtazamia Bwana; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. |
8. | Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu. |
9. | Nitaivumilia ghadhabu ya Bwana, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea teto langu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. |
10. | Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi Bwana, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu. |
11. | Ni siku ya kujengwa kuta zako! Siku hiyo mpaka utasongezwa mbali. |
12. | Siku hiyo watakujia kutoka Ashuru na miji ya Misri, na kutoka Misri mpaka huo Mto, na kutoka bahari hii mpaka bahari hii, na kutoka mlima huu mpaka mlima huu. |
13. | Hata hivyo nchi itakuwa ukiwa kwa sababu ya hao wakaao ndani yake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao. |
14. | Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. |
15. | Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. |
16. | Mataifa wataona, na kuzitahayarikia nguvu zao zote; wataweka mikono yao juu ya vinywa vyao, masikio yao yatakuwa na uziwi. |
17. | Watayaramba mavumbi kama nyoka, kama vitu vitambaavyo juu ya nchi watatoka katika mahali walimojificha, wakitetemeka; watakuja kwa Bwana, Mungu wetu, kwa hofu, nao wataogopa kwa sababu yako. |
18. | Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. |
19. | Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. |
20. | Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale. |
← Micah (7/7) |