← Micah (3/7) → |
1. | Nikasema, Tafadhali sikieni, enyi vichwa vya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli. Je! Haiwapasi ninyi kujua hukumu? |
2. | Ninyi mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi yao, na nyama mifupani mwao. |
3. | Naam, mnakula nyama ya watu wangu, na kuwachuna ngozi zao, na kuivunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa kutiwa chunguni, na kama nyama sufuriani. |
4. | Ndipo watakapomwomba Bwana, asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda mabaya kwa matendo yao. |
5. | Bwana asema hivi katika habari za manabii wanaowakosesha watu wangu; hao waumao kwa meno yao, na kulia, Amani; na mtu awaye yote asiyetia kitu vinywani mwao, wao humwandalia vita. |
6. | Kwa hiyo itakuwa usiku kwenu, msipate kuona maono; tena itakuwa giza kwenu, msiweze kubashiri; nalo jua litawachwea manabii, nao mchana utakuwa mweusi juu yao. |
7. | Na hao waonaji watatahayarika, na wenye kubashiri watafadhaika; naam, hao wote watajifunika midomo yao; kwa maana; hapana jawabu la Mungu. |
8. | Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa roho ya Bwana; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake. |
9. | Sikieni haya, tafadhali, enyi vichwa vya nyumba ya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli, mnaochukia hukumu, na kuipotosha adili. |
10. | Wanaijenga Sayuni kwa damu, na Yerusalemu kwa uovu. |
11. | Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea Bwana, na kusema, Je! Hayupo Bwana katikati yetu? Hapana neno baya lo lote litakalotufikia. |
12. | Basi, kwa ajili yenu, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu; na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni. |
← Micah (3/7) → |