← Mark (4/16) → |
1. | Akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari. |
2. | Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, |
3. | Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; |
4. | ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. |
5. | Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; |
6. | hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. |
7. | Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. |
8. | Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. |
9. | Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. |
10. | Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano. |
11. | Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano, |
12. | ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa. |
13. | Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? |
14. | Mpanzi huyo hulipanda neno. |
15. | Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. |
16. | Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; |
17. | ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. |
18. | Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, |
19. | na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. |
20. | Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia. |
21. | Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? |
22. | Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. |
23. | Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. |
24. | Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. |
25. | Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. |
26. | Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; |
27. | akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. |
28. | Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. |
29. | Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. |
30. | Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? |
31. | Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, |
32. | lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. |
33. | Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; |
34. | wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha. |
35. | Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. |
36. | Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. |
37. | Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. |
38. | Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? |
39. | Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. |
40. | Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? |
41. | Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii? |
← Mark (4/16) → |