← Mark (3/16) → |
1. | Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; |
2. | wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki. |
3. | Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati. |
4. | Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza. |
5. | Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. |
6. | Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza. |
7. | Naye Yesu akajitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, |
8. | na Yerusalemu, na Idumaya, na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. |
9. | Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. |
10. | Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. |
11. | Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. |
12. | Akawakataza sana, wasimdhihirishe. |
13. | Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. |
14. | Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, |
15. | tena wawe na amri ya kutoa pepo. |
16. | Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; |
17. | na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; |
18. | na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, |
19. | na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti. Kisha akaingia nyumbani. |
20. | Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. |
21. | Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili. |
22. | Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. |
23. | Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? |
24. | Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; |
25. | na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. |
26. | Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. |
27. | Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. |
28. | Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; |
29. | bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele, |
30. | kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu. |
31. | Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. |
32. | Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. |
33. | Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? |
34. | Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! |
35. | Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu. |
← Mark (3/16) → |