Mark (1/16) → |
1. | Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. |
2. | Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. |
3. | Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. |
4. | Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. |
5. | Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. |
6. | Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu. |
7. | Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. |
8. | Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. |
9. | Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. |
10. | Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; |
11. | na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. |
12. | Mara Roho akamtoa aende nyikani. |
13. | Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. |
14. | Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, |
15. | akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. |
16. | Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. |
17. | Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. |
18. | Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. |
19. | Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. |
20. | Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata. |
21. | Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. |
22. | Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. |
23. | Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, |
24. | akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? |
25. | Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. |
26. | Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. |
27. | Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! |
28. | Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. |
29. | Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. |
30. | Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. |
31. | Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. |
32. | Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. |
33. | Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. |
34. | Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. |
35. | Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. |
36. | Simoni na wenziwe wakamfuata; |
37. | nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. |
38. | Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea. |
39. | Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo. |
40. | Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. |
41. | Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. |
42. | Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. |
43. | Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, |
44. | akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. |
45. | Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali. |
Mark (1/16) → |