← Luke (9/24) → |
1. | Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. |
2. | Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. |
3. | Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. |
4. | Na nyumba yo yote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke mjini. |
5. | Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo, yakung'uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao. |
6. | Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri injili, na kupoza watu kila mahali. |
7. | Na Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu, |
8. | na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. |
9. | Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona. |
10. | Basi wale mitume waliporudi walimweleza mambo yote waliyoyatenda; akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida. |
11. | Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa. |
12. | Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu. |
13. | Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula. |
14. | Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini. |
15. | Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. |
16. | Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. |
17. | Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili. |
18. | Ikawa alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? |
19. | Wakamjibu wakisema, Yohana Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. |
20. | Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. |
21. | Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo; |
22. | akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. |
23. | Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. |
24. | Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. |
25. | Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe? |
26. | Kwa sababu kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. |
27. | Nami nawaambia kweli, Wapo katika hawa wanaosimama hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata wauone kwanza ufalme wa Mungu. |
28. | Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. |
29. | Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. |
30. | Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; |
31. | walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. |
32. | Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. |
33. | Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. |
34. | Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. |
35. | Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. |
36. | Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona. |
37. | Ikawa siku ya pili yake, waliposhuka mlimani, mkutano mkubwa ulikutana naye. |
38. | Na tazama, mtu mmoja katika mkutano alipaza sauti, akisema, Mwalimu, nakuomba umwangalie mwanangu; kwa kuwa yeye ni mwanangu pekee. |
39. | Na tazama, pepo humpagaa, naye mara hupiga kelele; tena humtia kifafa, huku anatokwa na povu, wala hamwachi ila kwa shida, akimchubua-chubua. |
40. | Nikawasihi wanafunzi wako wamtoe, wasiweze. |
41. | Yesu akajibu akasema, Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwachukulia hata lini? Mlete mwanao hapa. |
42. | Alipokuwa katika kumwendea, pepo akambwaga chini, akamtia kifafa. Yesu akamkemea pepo mchafu, akamponya mtoto, akamrudishia babaye. |
43. | Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu. Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake, |
44. | Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. |
45. | Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile. |
46. | Wakaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. |
47. | Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, |
48. | akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa. |
49. | Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. |
50. | Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu. |
51. | Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; |
52. | akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. |
53. | Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. |
54. | Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? |
55. | Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] |
56. | Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine. |
57. | Nao walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata ko kote utakakokwenda. |
58. | Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. |
59. | Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu. |
60. | Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. |
61. | Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. |
62. | Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu. |
← Luke (9/24) → |