← Luke (4/24) → |
1. | Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, |
2. | akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. |
3. | Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. |
4. | Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. |
5. | Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. |
6. | Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. |
7. | Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. |
8. | Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. |
9. | Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; |
10. | kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; |
11. | na ya kwamba, |
12. | Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. |
13. | Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda. |
14. | Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. |
15. | Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote. |
16. | Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. |
17. | Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, |
18. | Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, |
19. | Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. |
20. | Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. |
21. | Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. |
22. | Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? |
23. | Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe. |
24. | Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. |
25. | Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; |
26. | wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. |
27. | Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu. |
28. | Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. |
29. | Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; |
30. | lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake. |
31. | Akashuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; |
32. | wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo. |
33. | Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, |
34. | akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu. |
35. | Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. |
36. | Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka. |
37. | Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile. |
38. | Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. |
39. | Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. |
40. | Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. |
41. | Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. |
42. | Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. |
43. | Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. |
44. | Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya. |
← Luke (4/24) → |