← Luke (22/24) → |
1. | Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Sikukuu ya Pasaka. |
2. | Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. |
3. | Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. |
4. | Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. |
5. | Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. |
6. | Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano. |
7. | Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka. |
8. | Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila. |
9. | Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? |
10. | Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. |
11. | Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? |
12. | Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo. |
13. | Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. |
14. | Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. |
15. | Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; |
16. | kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. |
17. | Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; |
18. | Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja. |
19. | Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. |
20. | Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] |
21. | Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, |
22. | Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye! |
23. | Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo. |
24. | Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. |
25. | Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; |
26. | lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. |
27. | Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. |
28. | Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. |
29. | Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; |
30. | mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. |
31. | Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; |
32. | lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. |
33. | Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. |
34. | Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. |
35. | Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! |
36. | Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue. |
37. | Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. |
38. | Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi. |
39. | Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. |
40. | Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. |
41. | Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, |
42. | akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. |
43. | Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. |
44. | Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] |
45. | Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. |
46. | Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni. |
47. | Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Thenashara, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu. |
48. | Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu? |
49. | Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotukia, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga? |
50. | Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. |
51. | Yesu akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya. |
52. | Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maakida wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja wenye panga na marungu kama kukamata mnyang'anyi? |
53. | Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza. |
54. | Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. |
55. | Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. |
56. | Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. |
57. | Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. |
58. | Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. |
59. | Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. |
60. | Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika. |
61. | Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu. |
62. | Akatoka nje akalia kwa majonzi. |
63. | Na wale watu waliokuwa wakimshika Yesu walimfanyia dhihaka, wakampiga. |
64. | Wakamfunika macho, kisha wakamwuliza-uliza wakisema, Tabiri, ni nani aliyekupiga? |
65. | Wakamtolea na maneno mengine mengi ya kumtukana. |
66. | Hata kulipokucha, walikutanika jamii ya wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, wakamleta katika baraza yao, wakisema, |
67. | Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa. |
68. | Tena, nikiwauliza, hamtajibu. |
69. | Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi. |
70. | Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye. |
71. | Wakasema, Basi, tuna haja gani tena ya ushuhuda? Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake. |
← Luke (22/24) → |