← Luke (21/24) → |
1. | Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina. |
2. | Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. |
3. | Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; |
4. | maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo. |
5. | Na watu kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, alisema, |
6. | Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. |
7. | Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? |
8. | Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. |
9. | Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. |
10. | Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; |
11. | kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. |
12. | Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. |
13. | Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. |
14. | Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; |
15. | kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. |
16. | Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. |
17. | Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. |
18. | Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. |
19. | Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu. |
20. | Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. |
21. | Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. |
22. | Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa. |
23. | Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. |
24. | Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia. |
25. | Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; |
26. | watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. |
27. | Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. |
28. | Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia. |
29. | Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote. |
30. | Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. |
31. | Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu. |
32. | Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. |
33. | Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. |
34. | Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; |
35. | kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. |
36. | Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu. |
37. | Basi, kila mchana alikuwa akifundisha hekaluni, na usiku huenda kulala katika mlima uitwao wa Mizeituni. |
38. | Na watu wote walikuwa wakiamka mapema waende hekaluni ili kumsikiliza. |
← Luke (21/24) → |