← Luke (19/24) → |
1. | Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake. |
2. | Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. |
3. | Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. |
4. | Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. |
5. | Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. |
6. | Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. |
7. | Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. |
8. | Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. |
9. | Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. |
10. | Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. |
11. | Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. |
12. | Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. |
13. | Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. |
14. | Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. |
15. | Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. |
16. | Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. |
17. | Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. |
18. | Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida. |
19. | Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. |
20. | Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. |
21. | Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. |
22. | Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; |
23. | basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? |
24. | Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. |
25. | Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi. |
26. | Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho. |
27. | Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu. |
28. | Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu. |
29. | Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, |
30. | akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa. |
31. | Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. |
32. | Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. |
33. | Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda? |
34. | Wakasema, Bwana ana haja naye. |
35. | Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu. |
36. | Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. |
37. | Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, |
38. | wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. |
39. | Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. |
40. | Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele. |
41. | Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, |
42. | akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. |
43. | Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; |
44. | watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako. |
45. | Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, |
46. | akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. |
47. | Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; |
48. | wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza. |
← Luke (19/24) → |