← Luke (12/24) → |
1. | Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. |
2. | Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. |
3. | Basi, yo yote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari. |
4. | Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. |
5. | Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo. |
6. | Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. |
7. | Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi. |
8. | Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; |
9. | na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. |
10. | Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. |
11. | Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; |
12. | kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema. |
13. | Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. |
14. | Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? |
15. | Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. |
16. | Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; |
17. | akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. |
18. | Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. |
19. | Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. |
20. | Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? |
21. | Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. |
22. | Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini. |
23. | Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. |
24. | Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! |
25. | Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? |
26. | Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine? |
27. | Yatafakarini maua jinsi yameavyo; hayatendi kazi wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. |
28. | Basi, ikiwa Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatawatendea ninyi zaidi, enyi wa imani haba? |
29. | Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi, |
30. | kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo. |
31. | Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa. |
32. | Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. |
33. | Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. |
34. | Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu. |
35. | Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; |
36. | nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. |
37. | Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. |
38. | Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. |
39. | Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. |
40. | Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu. |
41. | Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia? |
42. | Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? |
43. | Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. |
44. | Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. |
45. | Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; |
46. | bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. |
47. | Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. |
48. | Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi. |
49. | Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? |
50. | Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! |
51. | Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. |
52. | Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. |
53. | Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu. |
54. | Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo. |
55. | Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo. |
56. | Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya? |
57. | Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki? |
58. | Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani. |
59. | Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho. |
← Luke (12/24) → |