← Lamentations (3/5) → |
1. | Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake. |
2. | Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala si katika nuru. |
3. | Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote. |
4. | Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu. |
5. | Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu. |
6. | Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani. |
7. | Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya mnyororo wangu mzito. |
8. | Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu. |
9. | Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu. |
10. | Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni. |
11. | Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua; Amenifanya ukiwa. |
12. | Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale. |
13. | Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake. |
14. | Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa. |
15. | Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga. |
16. | Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu. |
17. | Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa. |
18. | Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa Bwana. |
19. | Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo. |
20. | Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu. |
21. | Najikumbusha neno hili, Kwa hiyo nina matumaini. |
22. | Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi. |
23. | Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu. |
24. | Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye. |
25. | Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo. |
26. | Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. |
27. | Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake. |
28. | Na akae peke yake na kunyamaza kimya; Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake. |
29. | Na atie kinywa chake mavumbini; Ikiwa yamkini liko tumaini. |
30. | Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake; Ashibishwe mashutumu. |
31. | Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. |
32. | Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. |
33. | Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha. |
34. | Kuwaseta chini kwa miguu Wafungwa wote wa duniani, |
35. | Kuipotosha hukumu ya mtu Mbele zake Aliye juu, |
36. | Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa. |
37. | Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza? |
38. | Je! Katika kinywa chake Aliye juu Hayatoki maovu na mema? |
39. | Mbona anung'unika mwanadamu aliye hai Mtu akiadhibiwa kwa dhambi zake? |
40. | Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia Bwana tena. |
41. | Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni Mioyo yetu na mikono. |
42. | Sisi tumekosa na kuasi; Wewe hukusamehe. |
43. | Umetufunika kwa hasira na kutufuatia; Umeua, wala hukuona huruma. |
44. | Umejifunika nafsi yako kwa wingu, Maombi yetu yasipite. |
45. | Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa. |
46. | Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao. |
47. | Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu. |
48. | Jicho langu lachuruzika mito ya maji Kwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu. |
49. | Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi; |
50. | Hata Bwana atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni. |
51. | Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa sababu ya binti zote za mji wangu. |
52. | Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege; |
53. | Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu. |
54. | Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali. |
55. | Naliliitia jina lako, Bwana, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa. |
56. | Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu. |
57. | Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope. |
58. | Ee Bwana umenitetea mateto ya nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu. |
59. | Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee Bwana; Unihukumie neno langu. |
60. | Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu. |
61. | Ee Bwana, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu; |
62. | Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa. |
63. | Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi. |
64. | Utawalipa malipo, Ee Bwana, Sawasawa na kazi ya mikono yao. |
65. | Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao. |
66. | Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za Bwana. |
← Lamentations (3/5) → |