← John (7/21) → |
1. | Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. |
2. | Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. |
3. | Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. |
4. | Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. |
5. | Maana hata nduguze hawakumwamini. |
6. | Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo. |
7. | Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu. |
8. | Kweeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sikwei bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa haujatimia wakati wangu. |
9. | Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alikaa vivi hivi huko Galilaya. |
10. | Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. |
11. | Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule? |
12. | Kukawa na manung'uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano. |
13. | Walakini hakuna mtu aliyemtaja waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi. |
14. | Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alikwea kuingia hekaluni, akafundisha. |
15. | Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma? |
16. | Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka. |
17. | Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. |
18. | Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta utukufu wake aliyempeleka, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu. |
19. | Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta kuniua? |
20. | Mkutano wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua? |
21. | Yesu akajibu, akawaambia, Mimi nalitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia. |
22. | Musa aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi siku ya sabato humtahiri mtu. |
23. | Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nalimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato? |
24. | Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki. |
25. | Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? |
26. | Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? |
27. | Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. |
28. | Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. |
29. | Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma. |
30. | Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado. |
31. | Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu? |
32. | Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung'unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate. |
33. | Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka. |
34. | Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja. |
35. | Basi Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? Ati! Atakwenda kwa Utawanyiko wa Wayunani, na kuwafundisha Wayunani? |
36. | Ni neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja? |
37. | Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. |
38. | Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. |
39. | Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. |
40. | Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. |
41. | Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? |
42. | Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? |
43. | Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. |
44. | Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. |
45. | Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? |
46. | Wale watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena. |
47. | Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? |
48. | Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? |
49. | Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. |
50. | Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), |
51. | Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? |
52. | Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii. |
← John (7/21) → |