← John (11/21) → |
1. | Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. |
2. | Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. |
3. | Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. |
4. | Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. |
5. | Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. |
6. | Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. |
7. | Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena. |
8. | Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? |
9. | Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. |
10. | Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake. |
11. | Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. |
12. | Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. |
13. | Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. |
14. | Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa. |
15. | Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. |
16. | Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye. |
17. | Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. |
18. | Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; |
19. | na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. |
20. | Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. |
21. | Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. |
22. | Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. |
23. | Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. |
24. | Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. |
25. | Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; |
26. | naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? |
27. | Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni. |
28. | Naye alipokwisha kusema hayo, alikwenda zake; akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akisema, Mwalimu yupo anakuita. |
29. | Naye aliposikia, aliondoka upesi, akamwendea. |
30. | Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya kijiji; lakini alikuwa akalipo pale pale alipomlaki Martha. |
31. | Basi wale Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wakimfariji, walipomwona jinsi alivyoondoka upesi na kutoka, walimfuata; huku wakidhania ya kuwa anakwenda kaburini ili alie huko. |
32. | Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. |
33. | Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, |
34. | akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. |
35. | Yesu akalia machozi. |
36. | Basi Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. |
37. | Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife? |
38. | Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. |
39. | Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. |
40. | Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? |
41. | Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. |
42. | Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. |
43. | Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. |
44. | Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake. |
45. | Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini. |
46. | Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya Yesu. |
47. | Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. |
48. | Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu. |
49. | Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote; |
50. | wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. |
51. | Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo. |
52. | Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja. |
53. | Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua. |
54. | Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. |
55. | Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase. |
56. | Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana hali wamesimama hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii? |
57. | Na wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri ya kwamba mtu akimjua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata. |
← John (11/21) → |