← John (10/21) → |
1. | Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi. |
2. | Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. |
3. | Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. |
4. | Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. |
5. | Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. |
6. | Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia. |
7. | Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. |
8. | Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. |
9. | Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. |
10. | Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. |
11. | Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. |
12. | Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. |
13. | Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. |
14. | Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; |
15. | kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. |
16. | Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. |
17. | Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. |
18. | Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu. |
19. | Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo. |
20. | Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza? |
21. | Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je! Pepo aweza kuwafumbua macho vipofu? |
22. | Basi huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi. |
23. | Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani. |
24. | Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi. |
25. | Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. |
26. | Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu. |
27. | Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. |
28. | Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. |
29. | Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. |
30. | Mimi na Baba tu umoja. |
31. | Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige. |
32. | Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe? |
33. | Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu. |
34. | Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? |
35. | Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); |
36. | je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? |
37. | Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; |
38. | lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. |
39. | Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. |
40. | Akaenda zake tena ng'ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. |
41. | Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohana kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohana katika habari zake huyu yalikuwa kweli. |
42. | Nao wengi wakamwamini huko. |
← John (10/21) → |