← Job (33/42) → |
1. | Walakini, Ayubu, nakuomba usikilize matamko yangu, Ukayasikilize maneno yangu yote. |
2. | Tazama basi, nimefunua kinywa changu, Ulimi wangu umenena kinywani mwangu. |
3. | Maneno yangu yatatamka uelekevu wa moyo wangu; Na hayo niyajuayo midomo yangu itayanena kwa unyofu. |
4. | Roho ya Mungu imeniumba, Na pumzi za Mwenyezi hunipa uhai. |
5. | Kwamba waweza, nijibu; Yapange maneno yako sawasawa mbele yangu, usimame. |
6. | Tazama, mimi ni mbele ya Mungu kama ulivyo wewe; Mimi nami nilifinyangwa katika udongo. |
7. | Tazama, utisho wangu hautakutia hofu wewe, Wala sitakulemea kwa uzito. |
8. | Hakika umenena masikioni mwangu, Nami nimesikia sauti ya maneno yako, ukisema, |
9. | Mimi ni safi, sina makosa; Sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu; |
10. | Tazama, yuaona sababu za kufarakana nami, Hunihesabu kuwa ni adui yake; |
11. | Hunitia miguu yangu katika mkatale, Na mapito yangu yote huyapeleleza. |
12. | Tazama, nitakujibu, katika neno hili huna haki; Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu. |
13. | Nawe kwani kumnung'unikia, Kwa vile asivyotoa hesabu ya mambo yake yote? |
14. | Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. |
15. | Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; |
16. | Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, |
17. | Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; |
18. | Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga. |
19. | Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake; |
20. | Hata roho yake huchukia chakula, Na nafsi yake huchukia nyama nzuri. |
21. | Nyama ya mwili wake huliwa, isionekane; Na mifupa yake isiyoonekana yatokea nje. |
22. | Naam, nafsi yake inakaribia shimoni, Na uhai wake unakaribia waangamizi. |
23. | Kwamba akiwapo malaika pamoja naye, Mkalimani, mmoja katika elfu, Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo; |
24. | Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi. |
25. | Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto; Huzirudia siku za ujana wake; |
26. | Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia; Hata auone uso wake kwa furaha; Naye humrejezea mtu haki yake. |
27. | Yeye huimba mbele ya watu, na kusema, Mimi nimefanya dhambi, na kuyapotosha hayo yaliyoelekea, Wala sikulipizwa jambo hilo; |
28. | Yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni, Na uhai wangu utautazama mwanga. |
29. | Tazama, hayo yote ni Mungu anayeyafanya, Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu, |
30. | Ili kurudisha roho yake itoke shimoni, Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai. |
31. | Angalia sana, Ee Ayubu, unisikilize; Nyamaza, mimi nitasema. |
32. | Kama una neno la kusema, nijibu; Nena, kwani nataka kukuhesabia kuwa na haki. |
33. | Kama sivyo, unisikilize mimi; Nyamaza, nami nitakufunza hekima. |
← Job (33/42) → |