← Job (31/42) → |
1. | Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana? |
2. | Kwani sehemu ya Mungu itokayo juu ingekuwa nini, Na urithi wa Mwenyezi utokao juu? |
3. | Je! Siyo msiba kwa wasio haki, Na hasara kwao watendao uovu? |
4. | Je! Yeye hazioni njia zangu, Na kuzihesabu hatua zangu zote? |
5. | Kwamba nimetembea katika ubatili, Na mguu wangu umeukimbilia udanganyifu; |
6. | (Na nipimwe katika mizani iliyo sawasawa, Ili Mungu aujue uelekevu wangu); |
7. | Kwamba hatua yangu imekengeuka na kuiacha njia, Na moyo wangu kuyaandama macho yangu, Tena kwamba kipaku cho chote kimeshikamana na mikono yangu; |
8. | Basi na nipande, mwingine ale; Naam, mazao ya shamba langu na yang'olewe. |
9. | Kama moyo wangu ulishawishwa kwa mwanamke, Nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu; |
10. | Ndipo hapo mke wangu na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake. |
11. | Kwani hilo lingekuwa kosa kuu; Naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; |
12. | Kwa kuwa ni moto uteketezao hata Uharibifu, Nao ungeyang'oa maongeo yangu yote. |
13. | Kama nimeidharau daawa ya mtumishi wangu, au ya kijakazi changu, Waliposhindana nami; |
14. | Basi Mungu atakapoinuka nitafanya nini? Naye atakapozuru, nitamjibuje? |
15. | Je! Huyo aliyenifanya mimi ndani ya tumbo, siye aliyemfanya na yeye? Si yeye mmoja aliyetufinyanga tumboni? |
16. | Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, Au kama nimeyatia kiwi macho ya mwanamke mjane; |
17. | Au kama nimekula tonge langu peke yangu, Mayatima wasipate kulila; |
18. | (La, tangu ujana wangu alikua pamoja nami kama kwa baba; Nami nimekuwa ni kiongozi cha mjane tangu tumbo la mamangu); |
19. | Ikiwa nimemwona mtu kuangamia kwa kukosa nguo, Au wahitaji kukosa mavazi; |
20. | Ikiwa viuno vyake havikunibarikia, Au kama hakupata moto kwa manyoya ya kondoo zangu; |
21. | Ikiwa nimewainulia mayatima mkono, Nilipoona msaada wangu langoni; |
22. | Basi bega langu na lianguke kutoka mahali pake, Na mkono wangu uvunjike mfupani mwake. |
23. | Kwani msiba utokao kwa Mungu ulikuwa na kitisho kwangu, Na kwa sababu ya ukuu wake sikuweza kufanya neno. |
24. | Ikiwa nimeifanya dhahabu kuwa tumaini langu, Na kuiambia dhahabu safi, Wewe u tegemeo langu; |
25. | Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi; |
26. | Kama nililitazama jua lilipoangaza, Au mwezi ukiendelea katika kung'aa; |
27. | Na moyo wangu umeshawishwa kwa siri, Na midomo yangu imeubusu mkono wangu; |
28. | Hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; Kwani ningemwambia uongo Mungu aliye juu. |
29. | Kama nilifurahi kwa kuangamia kwake huyo aliyenichukia, Au kujitukuza alipopatikana na maovu; |
30. | (Naam, sikukiacha kinywa changu kufanya dhambi Kwa kuutaka uhai wake kwa kuapiza); |
31. | Kama watu wa hemani mwangu hawakunena, Ni nani awezaye kumpata mtu asiyeshibishwa na yeye kwa nyama? |
32. | Mgeni hakulala njiani; Lakini nilimfungulia msafiri milango yangu; |
33. | Ikiwa kama mwanadamu nimeyafunika makosa yangu, Kwa kuuficha uovu wangu kifuani mwangu; |
34. | Kwa sababu niliwaogopa mkutano mkubwa, Na dharau la jamaa lilinitia hofu, Hata nilinyamaa kimya, nisitoke mlangoni- |
35. | Laiti ningekuwa na mtu wa kunisikia! (Tazama, sahihi yangu ni hii, Mwenyezi na anijibu); Laiti ningekuwa na hayo mashitaka yaliyoandikwa na adui yangu! |
36. | Hakika ningeyachukua mabegani; Ningejifungia mfano wa kilemba. |
37. | Ningemwambia hesabu ya hatua zangu Ningemkaribia kama vile mkuu. |
38. | Kama nchi yangu yalia juu yangu, Na matuta yake hulia pamoja; |
39. | Kama nimeyala matunda yake pasipo kulipa, Au kama nimewafanya wenyewe kupotewa na uhai; |
40. | Miiba na imee badala ya ngano, Na magugu badala ya shayiri. Maneno ya Ayubu yamekoma hapa. |
← Job (31/42) → |