← Job (30/42) → |
1. | Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanyia mzaha, Ambao baba zao niliwadharau hata kuwaweka na mbwa wa kundi langu. |
2. | Naam, uwezo wa mikono yao utanifaa nini? Watu ambao nguvu zao zimekoma. |
3. | Wamekonda kwa uhitaji na njaa; Huguguna nchi kavu, penye giza la ukiwa na uharibifu. |
4. | Hung'oa mboga ya chumvi kwenye kichaka; Na mizizi ya mretemu ni chakula chao. |
5. | Hufukuzwa watoke kati ya watu; Huwapigia kelele kama kumpigia mwivi. |
6. | Lazima hukaa katika mianya ya mabonde, Katika mashimo ya nchi na ya majabali. |
7. | Hulia kama punda vichakani; Hukusanyika chini ya upupu. |
8. | Wao ni wana wa wapumbavu, naam, watoto wa wahuni; Walifukuzwa kwa mijeledi watoke katika nchi. |
9. | Na sasa mimi nimekuwa wimbo wao, Naam, nimekuwa simo kwao. |
10. | Wao hunichukia, na kujitenga nami, Hawaachi kunitemea mate usoni. |
11. | Kwani ameilegeza kamba yake, na kunitesa, Wala hawajizuii tena mbele yangu. |
12. | Kwa mkono wangu wa kuume huinuka kundi; Huisukuma miguu yangu kando, Na kunipandishia njia zao za uharibifu. |
13. | Waiharibu njia yangu, Wauzidisha msiba wangu, Watu wasio na msaidizi. |
14. | Wanijilia kama wapitao katika ufa mpana; Katikati ya magofu wanishambulia. |
15. | Vitisho vimenigeukia; Huifukuza heshima yangu kama upepo; Na kufanikiwa kwangu kumepita kama wingu. |
16. | Sasa nafsi yangu inamwagika ndani yangu; Siku za mateso zimenishika. |
17. | Wakati wa usiku mifupa yangu huchomeka ndani yangu, Na maumivu yanayonitafuna hayapumziki. |
18. | Kwa ugonjwa wangu kuwa na nguvu nyingi Mavazi yangu yameharibika; Hunikaza kama shingo ya kanzu yangu. |
19. | Yeye amenibwaga topeni, Nami nimekuwa kama mavumbi na majivu. |
20. | Nakulilia wewe, wala huniitikii; Nasimama, nawe wanitazama tu. |
21. | Wewe umegeuka kuwa mkali kwangu; Nawe waniudhi kwa uweza wa mkono wako. |
22. | Waniinua juu hata upeponi, na kunipandisha juu yake; Nawe waniyeyusha katika dhoruba. |
23. | Kwani najua kuwa utanileta hata kifoni, Niifikilie nyumba waliyoandikiwa wenye uhai wote. |
24. | Je! Mtu katika kuanguka kwake hanyoshi mkono? Na kulilia msaada katika msiba wake? |
25. | Je! Mimi sikulia kwa ajili ya huyo aliyekuwa katika taabu? Nafsi yangu, je! Haikusononeka kwa ajili ya wahitaji? |
26. | Hapo nilipotazamia mema, ndipo yakaja mabaya; Nami nilipongojea mwanga, likaja giza. |
27. | Matumbo yangu yatokota, wala hayaachi; Siku za taabu zimenijilia. |
28. | Naenda nikiomboleza pasipo jua; Nasimama katika mkutano, na kuulilia msaada. |
29. | Mimi ni ndugu yao mbwa-mwitu, Ni mwenzao mbuni. |
30. | Ngozi yangu ni nyeusi, nayo yanitoka, Na mifupa yangu imeteketea kwa hari. |
31. | Kwa hiyo kinanda changu kimegeuzwa kuwa maombolezo, Na filimbi yangu kuwa sauti yao waliao. |
← Job (30/42) → |