← Job (3/42) → |
1. | Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. |
2. | Ayubu akajibu, na kusema; |
3. | Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. |
4. | Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. |
5. | Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. |
6. | Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. |
7. | Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. |
8. | Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani. |
9. | Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi; |
10. | Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni. |
11. | Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? |
12. | Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? |
13. | Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; |
14. | Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; |
15. | Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao; |
16. | Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. |
17. | Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika |
18. | Huko wafungwa waona raha pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi. |
19. | Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yu huru kwa bwana wake. |
20. | Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; |
21. | Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika; |
22. | Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? |
23. | Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo? |
24. | Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. |
25. | Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia. |
26. | Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu. |
← Job (3/42) → |