← Job (20/42) → |
1. | Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu, na kusema, |
2. | Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu, Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu. |
3. | Nimesikia maonyo yanayonitahayarisha, Nayo roho ya ufahamu wangu hunijibu. |
4. | Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale, Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi, |
5. | Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu? |
6. | Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni, Na kichwa chake kufikilia mawinguni; |
7. | Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe; Hao waliomwona watasema, Yuko wapi? |
8. | Ataruka mfano wa ndoto, asionekane; Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku, |
9. | Jicho lililomwona halitamwona tena; Wala mahali pake hapatamtazama tena. |
10. | Watoto wake watataka fadhili kwa maskini, Na mikono yake itarudisha mali yake. |
11. | Mifupa yake imejaa ujana wake, Lakini utalala nchi naye mavumbini. |
12. | Ingawa uovu una tamu kinywani mwake, Ingawa auficha chini ya ulimi wake; |
13. | Ingawa auhurumia, asikubali kuuacha uende zake. Lakini akaushika vivyo kinywani mwake; |
14. | Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika, Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake. |
15. | Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake. |
16. | Ataamwa sumu ya majoka; Na ulimi wa fira utamwua. |
17. | Hataiangalia hiyo mito ya maji, Vile vijito vilivyojaa asali na siagi. |
18. | Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze; Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi. |
19. | Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini; Amenyang'anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga. |
20. | Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake, Hataponya cho chote katika hicho alichokifurahia. |
21. | Hakikusalia kitu asichokula; Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu. |
22. | Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki; Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia. |
23. | Hapo atakapo kulijaza tumbo lake, Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake, Na kuunyesha juu yake akiwa anakula. |
24. | Ataikimbia silaha ya chuma, Na uta wa shaba utamchoma kwa pili. |
25. | Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake; Naam, ncha ing'aayo yatoka katika nyongo yake; Vitisho viko juu yake. |
26. | Giza lote linawekwa kwa ajili ya hazina zake; Moto ambao haukuvuviwa na mtu utamla; Utayateketeza yaliyosalia hemani mwake. |
27. | Mbingu zitafunua wazi uovu wake, Nayo nchi itainuka kinyume chake. |
28. | Maongeo ya nyumba yake yataondoka, Yatamwagika mbali katika siku ya ghadhabu zake. |
29. | Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu, Na urithi aliowekewa na Mungu. |
← Job (20/42) → |