← Job (18/42) → |
1. | Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema, |
2. | Je! Hata lini utayategea maneno mitambo? Fikiri, kisha baadaye tutanena. |
3. | Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani, Tena kuwa wanajisi machoni pako? |
4. | Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako, Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe? Au jabali litaondolewa mahali pake? |
5. | Naam, mwanga wa waovu utazimika, Wala mwali wa moto wake hautang'aa. |
6. | Mwanga hemani mwake utakuwa giza, Nayo taa iliyo juu yake itazimishwa. |
7. | Hatua zake za nguvu zitasongwa, Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini. |
8. | Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe, Naye huenda juu ya matanzi. |
9. | Tanzi litamshika kisigino chake, Na mtambo utamgwia. |
10. | Amefichiwa tanzi chini, Na mtego amewekewa njiani. |
11. | Matisho yatamtia hofu pande zote, Na kumfukuza karibu na visigino vyake. |
12. | Nguvu zake zitaliwa na njaa, Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake. |
13. | Utakula via vya mwili wake, Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake. |
14. | Atang'olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho. |
15. | Ambacho si chake kitakaa katika hema yake; Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake. |
16. | Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa. |
17. | Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani. |
18. | Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani, Na kufukuzwa atoke duniani. |
19. | Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake, Wala hatasalia mtu hapo alipokaa. |
20. | Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake, Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu. |
21. | Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu. |
← Job (18/42) → |