← Job (16/42) → |
1. | Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, |
2. | Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha. |
3. | Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu? |
4. | Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu. |
5. | Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na utuzo wa midomo yangu ungetuliza. |
6. | Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani? |
7. | Lakini sasa amenichokesha; Jamii yangu yote umeifanya ukiwa. |
8. | Umenishika sana, ni ushahidi juu yangu; Na kukonda kwangu kwaniinukia, kwanishuhudia usoni pangu. |
9. | Amenirarua katika ghadhabu zake, na kunionea; Amesaga-saga meno juu yangu; Mtesi wangu hunikazia macho makali. |
10. | Wamenifumbulia vinywa vyao; Wamenipiga shavuni kwa kunitukana; Hujikutanisha pamoja juu yangu. |
11. | Mungu amenitia kwa hao wapotovu, Na kunitupa mikononi mwao waovu. |
12. | Nilikuwa katika raha, naye akanivunja-vunja; Naam, amenishika shingo, na kuniponda; Tena amenisimamisha niwe shabaha yake. |
13. | Wapigaji wake wa mishale hunizingira kotekote, Hunipasua viuno vyangu, asinihurumie; Nyonga zangu amezimwaga juu ya nchi. |
14. | Hunivunja kwa uvunjifu juu ya uvunjifu; Hunishambulia mfano wa jitu shujaa. |
15. | Nimeshona nguo ya magunia juu ya mwili wangu, Na pembe yangu nimeidhili uvumbini. |
16. | Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu li katika kope zangu; |
17. | Ijapokuwa hapana jeuri mikononi mwangu, Na kuomba kwangu ni safi. |
18. | Ee nchi, usiifunike damu yangu, Na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika. |
19. | Hata sasa, tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu. |
20. | Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi; |
21. | Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, Amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake. |
22. | Kwani ikiisha pita miaka michache, Nitakwenda njia hiyo ambayo sitarudi tena. |
← Job (16/42) → |