← Jeremiah (50/52) → |
1. | Neno hili ndilo alilosema Bwana, katika habari za Babeli, na katika habari za Wakaldayo, kwa kinywa cha Yeremia, nabii. |
2. | Tangazeni katika mataifa, Mkahubiri na kutweka bendera; Hubirini, msifiche, semeni, Babeli umetwaliwa! Beli amefedheheka; Merodaki amefadhaika; Sanamu zake zimeaibishwa, Vinyago vyake vimefadhaika. |
3. | Maana toka kaskazini taifa linakuja juu yake, litakaloifanya nchi yake kuwa ukiwa; wala hapana mtu atakayekaa humo; wamekimbia, wamekwenda zao, mwanadamu na mnyama pia. |
4. | Katika siku hizo, na wakati huo, asema Bwana, wana wa Israeli watakuja, wao na wana wa Yuda pamoja; Wataendelea njiani mwao wakilia, nao watamtafuta Bwana, Mungu wao. |
5. | Watauliza habari za Sayuni, na nyuso zao zitaelekea huko, wakisema, Njoni ninyi, mjiunge na Bwana, kwa agano la milele ambalo halitasahauliwa. |
6. | Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika. |
7. | Watu wote waliowaona wamewala; na adui zao walisema, Sisi hatuna hatia, kwa kuwa hao wametenda dhambi juu ya Bwana, aliye kao la haki, yaani, Bwana, tumaini la baba zao. |
8. | Kimbieni kutoka kati ya Babeli, mkatoke katika nchi ya Wakaldayo, mkawe kama mabeberu mbele ya makundi. |
9. | Kwa maana juu ya Babeli nitaamsha na kuleta kusanyiko la mataifa makubwa, toka nchi ya kaskazini; nao watajipanga juu yake; kutoka huko atatwaliwa; mishale yao itakuwa kama ya mtu shujaa aliye stadi; hapana hata mmoja utakaorudi bure. |
10. | Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema Bwana. |
11. | Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmewanda kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu; |
12. | mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika. |
13. | Kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote. |
14. | Jipangeni juu ya Babeli pande zote, Ninyi nyote mpindao upinde; Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja; Kwa maana amemtenda Bwana dhambi. |
15. | Mpigieni kelele pande zote; amejitoa; Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa; Kwa maana ni kisasi cha Bwana; mlipizeni kisasi; Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye. |
16. | Mpanzi mkatilie mbali na Babeli, Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno; Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao, Watageuka kila mtu kwa watu wake, Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake. |
17. | Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadreza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake. |
18. | Basi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, mimi nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru. |
19. | Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi. |
20. | Katika siku hizo na wakati huo, asema Bwana, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki. |
21. | Panda juu ya nchi ya Merathaimu, naam, juu yake, na juu yao wakaao Pekodi; ua, ukaangamize nyuma yao, asema Bwana, ukatende kama nilivyokuagiza, yote pia. |
22. | Pana mshindo wa vita katika nchi, Mshindo wa uharibifu mkuu. |
23. | Imekuwaje nyundo ya dunia yote Kukatiliwa mbali na kuvunjwa? Imekuwaje Babeli kuwa ukiwa Katikati ya mataifa? |
24. | Nimekutegea mtego, Ee Babeli, nawe ukanaswa, nawe ulikuwa huna habari; umeonekana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana na Bwana. |
25. | Bwana amefungua akiba yake ya silaha, naye amezitoa silaha za ghadhabu yake; maana Bwana, Bwana wa majeshi, ana kazi atakayofanya katika nchi ya Wakaldayo. |
26. | Njoni juu yake toka mpaka ulio mbali; Zifungueni ghala zake; Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa; Msimsazie kitu cho chote. |
27. | Wachinjeni mafahali wake wote; Na watelemkie machinjoni; Ole wao! Maana siku yao imewadia, Wakati wa kujiliwa kwao. |
28. | Sauti yao wakimbiao na kuokoka, Kutoka katika nchi ya Babeli, Ili kutangaza Sayuni kisasi cha Bwana, Mungu wetu, Kisasi cha hekalu lake. |
29. | Waiteni wapiga mishale juu ya Babeli, Naam, wote waupindao upinde; Pangeni hema kumzunguka pande zote; Ili asiokoke hata mtu mmoja wao; Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake; Mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda; Kwa sababu amefanya kiburi juu ya Bwana, Juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli. |
30. | Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema Bwana. |
31. | Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, Bwana wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia. |
32. | Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote. |
33. | Bwana wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha. |
34. | Mkombozi wao ni hodari; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli. |
35. | Upanga u juu ya Wakaldayo, asema Bwana, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima. |
36. | Upanga u juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga u juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika. |
37. | Upanga u juu ya farasi zao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa. |
38. | Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu. |
39. | Basi, wanyama wakali wa jangwani, pamoja na mbwa-mwitu, watakaa huko, na mbuni watakaa ndani yake; wala haitakaliwa na watu milele; wala hapana mtu atakayekaa huko tangu kizazi hata kizazi. |
40. | Kama vile vilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema Bwana; kadhalika hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama wageni wakaavyo. |
41. | Angalia, watu wanakuja watokao kaskazini; na taifa kubwa, na wafalme wengi wataamshwa toka pande za mwisho za dunia. |
42. | Wanashika upinde na mkuki; Ni wakatili, hawana huruma; Sauti yao inanguruma kama bahari, Nao wamepanda farasi; Kila mmoja amejipanga kama aendaye vitani, Juu yako, Ee binti Babeli. |
43. | Mfalme wa Babeli amesikia habari zao, Na mikono yake imekuwa dhaifu; Dhiki imemshika, na maumivu, Kama ya mwanamke katika utungu wake. |
44. | Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu? |
45. | Basi, lisikieni shauri la Bwana, Alilolifanya juu ya Babeli; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu ya nchi ya Wakaldayo. Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao. |
46. | Kwa mshindo wa kutwaliwa Babeli nchi yatetemeka, Na kilio chake chasikiwa katika mataifa. |
← Jeremiah (50/52) → |