← Jeremiah (39/52) → |
1. | Hata ikawa, Yerusalemu ulipotwaliwa, (katika mwaka wa kenda wa Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na jeshi lake lote, wakaja juu ya Yerusalemu, wakauhusuru; |
2. | katika mwaka wa kumi na mmoja wa Sedekia, mwezi wa nne, siku ya kenda ya mwezi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa;) |
3. | wakuu wote wa mfalme wa Babeli wakaingia, wakaketi katika lango la katikati, yaani, Nergal-Shareza, mnyweshaji, Nebu-Sarseki, mkuu wa matowashi, Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu, |
4. | Ikawa Sedekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa vita walipowaona, ndipo wakakimbia, wakatoka mjini usiku, kwa njia ya bustani ya mfalme, kwa lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili; naye akatoka kwa njia ya Araba. |
5. | Lakini jeshi la Wakaldayo wakawafuatia, wakampata Sedekia katika nchi tambarare ya Yeriko; nao walipomkamata, wakamleta kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, huko Ribla katika nchi ya Hamathi, naye akatoa hukumu juu yake. |
6. | Ndipo mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia huko Ribla mbele ya macho yake; pia mfalme wa Babeli akawaua wakuu wote wa Yuda. |
7. | Pamoja na hayo akampofusha macho Sedekia, akamfunga kwa pingu ili amchukue mpaka Babeli. |
8. | Nao Wakaldayo wakaiteketeza nyumba ya mfalme, na nyumba za watu kwa moto, wakazibomoa kuta za Yerusalemu. |
9. | Basi, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka mabaki ya watu waliosalia katika mji mpaka Babeli, na hao pia waliouacha mji na kujiunga naye, na mabaki ya watu waliosalia. |
10. | Lakini Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawaacha baadhi ya maskini wa watu, waliokuwa hawana kitu, katika nchi ya Yuda, akawapa mashamba ya mizabibu na makonde wakati uo huo. |
11. | Basi Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamwagiza Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, katika habari za Yeremia, akisema, |
12. | Mtwae, umtunze sana, wala usimtende neno baya lo lote; lakini umtendee kama atakavyokuambia. |
13. | Basi Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, na Nebu-Shazbani, mkuu wa matowashi, na Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu, |
14. | wakatuma watu wakamwondoa Yeremia katika uwanda wa walinzi, wakamweka katika mikono ya Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ili ampeleke nyumbani kwake; basi akakaa pamoja na hao watu. |
15. | Basi neno la Bwana likamjia Yeremia, wakati ule alipokuwa amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema, |
16. | Haya! Enenda ukaseme na Ebedmeleki, Mkushi, kusema, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaupatiliza mji huu maneno yangu kwa mabaya, wala si kwa mema; nayo yatatimizwa mbele yako katika siku hiyo. |
17. | Lakini nitakuokoa wewe katika siku hiyo, asema Bwana; wala hutatiwa katika mikono ya watu wale unaowaogopa. |
18. | Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema Bwana. |
← Jeremiah (39/52) → |