← Jeremiah (30/52) → |
1. | Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, |
2. | Bwana Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia. |
3. | Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema Bwana; nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki. |
4. | Na haya ndiyo maneno aliyosema Bwana, katika habari za Israeli, na katika habari za Yuda. |
5. | Maana Bwana asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani. |
6. | Ulizeni sasa, mkaone kwamba mwanamume aona utungu wa uzazi; mbona, basi, ninaona kila mtu anaweka mikono yake viunoni, kama mwanamke aliye na utungu, na nyuso zote zimegeuka rangi. |
7. | Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo. |
8. | Na itakuwa katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena; |
9. | bali watamtumikia Bwana, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao. |
10. | Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema Bwana; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu. |
11. | Maana mimi ni pamoja nawe, asema Bwana, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu. |
12. | Maana Bwana asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa. |
13. | Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo. |
14. | Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zilikuwa zimeongezeka. |
15. | Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya. |
16. | Basi, watu wote wakulao wataliwa; na adui zako wote watakwenda kufungwa; kila mmoja wao; na hao waliokuteka nyara watatekwa; na wote waliokuwinda nitawafanya kuwa mawindo. |
17. | Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye. |
18. | Bwana asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake. |
19. | Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge. |
20. | Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wawaoneao. |
21. | Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema Bwana. |
22. | Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. |
23. | Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea tufani ya kudumu; itawaangukia waovu vichwani. |
24. | Hasira kali ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kutenda, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtayafahamu haya. |
← Jeremiah (30/52) → |