← Jeremiah (13/52) → |
1. | Bwana akaniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. |
2. | Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la Bwana, nikajivika viunoni. |
3. | Nalo neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema, |
4. | Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. |
5. | Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama Bwana alivyoniamuru. |
6. | Hata ikawa, baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. |
7. | Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote. |
8. | Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema, |
9. | Bwana asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. |
10. | Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote. |
11. | Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema Bwana; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia. |
12. | Basi utawaambia neno hili, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai? |
13. | Ndipo utakapowaambia, Bwana asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu. |
14. | Nitawagonganisha, mtu na mwenzake, naam, baba za watu na watoto wao pamoja, asema Bwana; sitahurumia, wala sitaachilia, wala sitarehemu, hata nisiwaangamize. |
15. | Sikilizeni ninyi, kategeni masikio yenu; msifanye kiburi; maana Bwana amenena. |
16. | Mtukuzeni Bwana, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, na kabla miguu yenu haijakwaa juu ya milima yenye giza; na wakati mnapoitazamia nuru, kabla hajaigeuza kuwa kivuli cha mauti, na giza nene. |
17. | Bali kama hamtaki kusikia, roho yangu italia kwa siri, kwa sababu ya kiburi chenu; na jicho langu litalia sana na kutoka machozi mengi, kwa kuwa kundi la Bwana limechukuliwa hali ya kufungwa. |
18. | Mwambie mfalme, na mama ya mfalme, Nyenyekeeni na kuketi chini; Kwa maana vilemba vyenu vimeshuka, naam, taji ya utukufu wenu. |
19. | Miji ya Negebu imefungwa malango yake, wala hapana mtu wa kuyafungua; Yuda amechukuliwa hali ya kufungwa; amechukuliwa kabisa hali ya kufungwa. |
20. | Inua macho yako, Ee Yerusalemu, ukawatazame hawa wanaokuja kutoka kaskazini; liko wapi kundi lako ulilopewa, kundi lile zuri? |
21. | Utasema nini wewe, atakapowaweka rafiki zako kuwa kichwa juu yako, ikiwa wewe mwenyewe umewafundisha kuwa juu yako? Je! Huzuni haitakushika, kama utungu wa mwanamke aliye katika kuzaa? |
22. | Nawe ukisema moyoni mwako, Mbona mambo haya yamenipata mimi? Ni kwa sababu ya wingi wa uovu wako, marinda yako yamefunuliwa, na visigino vya miguu yako vimeumia. |
23. | Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya. |
24. | Kwa sababu hiyo nitawatawanya, kama makapi yapitayo, kwa upepo wa jangwani. |
25. | Hiyo ndiyo kura yako, fungu lako ulilopimiwa na mimi, asema Bwana; kwa kuwa umenisahau, na kuutumainia uongo. |
26. | Kwa ajili ya hayo, mimi nami nitayafunua marinda yako mbele ya uso wako, na aibu yako itaonekana. |
27. | Nimeona machukizo yako, naam, uzinifu wako, na ubembe wako, na uasherati wa ukahaba wako, juu ya milima katika mashamba. Ole wako, Ee Yerusalemu! Hutaki kutakaswa; mambo hayo yataendelea hata lini? |
← Jeremiah (13/52) → |